Oscar Pistorius
Reeva Steenkamp
Kesi kamili inayomkabili nyota huyo inaweza kuanza kusikilizwa miezi kadhaa ijayo, na Pistorius nyota wa Olimpiki na Paralimpiki, ambaye hana miguu yote miwili, anakabiliwa na hatari ya kifungo cha maisha kama akikutwa na hatia ya mauaji
JOHNNESBURG, South Africa
MWANARIADHA nyota wa mbio za walemavu Oscar Pistorius, hatimaye leo Ijumaa mchana ameachiwa kwa dhamana, kutokana na kesi ya mauaji ya mpenzi wake inayomkabili.
Umauzi wa Pistorius kupewa dhamana ulitolewa na Jaji Desmond Nair, na kuamsha furaha miongoni mwa wanafamilia wa Pistorius na mashabiki wake ndani na nje ya Mahakama ya jijini Pretoria, huku mwenyewe akiwa amesimama imara kama aliyenyimwa dhamana hiyo.
Kuachiwa kwa Pistorius kunafuatia wiki nzima ya usikilizaji wa maelezo ya namna mwanariadha huyo alivyompiga risasi na kumuua mpenzi wake Reeva Steenkamp wakiwa katika jumba lao la kifahari, asubuhi ya Siku ya Wapendao Februari 14.
Waendesha mashtaka wamesema Pistorius, 26, anakabiliwa na kesi ya kujibu kutokana na kupiga risasi nne kwenye mlango wa bafu ukiwa umefungwa, huku mpenzi wake akiwa ndani. Steenkamp, 29, alikutwa na majeraha ya risasi katika kichwa chake, mkononi na kwenye nyonga.
Upande unaomtetea Pistorius umeendelea kusisitiza kuwa mkali huyo alimuua mkewe kimakosa, wakisema alifanya hivyo kutokana na kuhisi kuwa amevamia na jambazi, wakataka apewe dhamana kuweza kujiandaa, kuikabili kesi hiyo iliyoteka hisia za wengi duniani.
Kesi kamili inayomkabili nyota huyo inaweza kuanza kusikilizwa miezi kadhaa ijayo, na Pistorius nyota wa Olimpiki na Paralimpiki, ambaye hana miguu yote miwili, anakabiliwa na hatari ya kifungo cha maisha kama akikutwa na hatia ya mauaji.
Dhamana hii imefungua milango ya matumaini miongoni mwa wanafamilia na mashabiki wake, kuwa anaweza kushinda vita ya kuepuka kifungo cha maisha.