skip to main |
skip to sidebar
TAHADHARI KWA WANAOPENDA KUNUNUA "MALAYA"......DODOMA WAMENASWA WAKIWA NA ARVAs
WANAWAKE
watatu raia wa Rwanda wanaosadikiwa kuendesha biashara ya ukahaba mjini
Dodoma wamekamatwa na kupewa siku tatu kuondoka nchini, huku wawili
kati yao wakikutwa na vidonge vya kupunguza makali ya virusi ya Ukimwi
(ARVs).
Kukamatwa kwa wanawake hao ambao ni Esperance Hagenimana
(28), Vestina Zaninika (27) na Ziada Mukamurera (25), kunafuatia mmoja
wao Esperance kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi kuwa alikuwa
ameibiwa fedha taslimu Sh 800,000 na hati ya kusafiria.
Lakini,
Polisi walipofika nyumba ya kulala wageni waliyofikia iliyopo eneo la
Area D walikuta wanawake wengine wawili ambao walikuwa wakikaa chumba
kimoja na Esperance.
Uchunguzi wa Polisi ulibaini kuwa mwanamke huyo
hakuibiwa na kubaini wote si raia wa Tanzania. Hata hivyo kilikosekana
kifungu cha kuwashitaki ndipo waliamua kupeleka sakata hilo Uhamiaji ili
liweze kushughulikiwa.
Kulingana na maelezo yao, Esperance
alitangulia kuja nchini kisha kuwaita wenzake ambao ilikuwa ni mara ya
kwanza kuja nchini, lakini hata hivyo alisema kuwa, kumekuwa na makundi
ya wanawake kutoka Rwanda wanaokuja nchini kipindi cha Bunge na hata
mwaka jana kuna kundi lilikuja wakati wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya
Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kulingana na uchunguzi
uliofanywa na Uhamiaji, wanawake hao waliingia nchini na kujitambulisha
kuwa walikuja Dodoma kufanya biashara ya vitenge, lakini hawakuwa hata
na kitenge kimoja ambacho kingeweza kuwaonesha kuwa walikuwa wakifanya
biashara hiyo.
Juhudi hizo za Uhamiaji zinadaiwa kuwafikisha hadi
klabu moja maarufu ya usiku iliyopo eneo la Area D ambapo walinzi wa
Kimasai walikiri kuwafahamu wanawake hao na walikuwa wakiwafuata nyumba
ya wageni waliyofikia kama mtu alikuwa akiwahitaji na walikuwa na ni
wateja wa klabu hiyo ya usiku.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Naibu
Kamishna wa Uhamiaji, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Dodoma, Norah Massawe
alikiri kukamatwa kwa wanawake hao na polisi na kukabidhiwa Uhamiaji.
Alisema
mwanzoni wanawake hao walidai kuwa walikuja Dodoma kwa ajili ya kununua
vitenge kwa ajili ya biashara na waliposhikiliwa na Polisi kwa siku
kadhaa waliomba kurudishwa nchini kwao.
Alisema wawili kati yao walikutwa wakiwa na vidonge vya ARVs, lakini haijafahamika moja kwa moja kama walikuwa wagonjwa au la.
“Siwezi
kusema walikuwa ni makahaba bali wanahisiwa hivyo kutokana na biashara
waliyosema wanafanya kutoeleweka na hata maelezo ya walinzi wa klabu ya
usiku kuwa walitambuliwa kama wateja wao, kwa kweli hilo siwezi
kulithibitisha,” alisema.
Aliwataka wananchi kuwa makini na watu
wasiowafahamu kwani hivi sasa Mkoa wa Dodoma umekuwa na mwingiliano
mkubwa wa watu hasa katika kipindi cha Bunge.
Mwandishi wa habari
hizi, alimtafuta Mratibu wa Ukimwi Mkoa wa Dodoma, Audrey Njelekela
ambaye alisema kuwa, wamekuwa wakitoa elimu kuanzia ngazi ya Mkoa hadi
mtaa ambapo kuna timu ya Mkoa ya Ukimwi na hata kwenye halmashauri kuna
waratibu ambao wamekuwa akitoa elimu juu ya masuala mbalimbali
yanayohusu Ukimwi.
Alisema kuwa kwa sasa kiwango cha maambukizi kwa
Mkoa wa Dodoma ni asilimia 2.9 kwa takwimu za mwaka 2011 na 2012
ikilinganisha na takwimu za mwaka 2007 hadi 2008 ambapo kiwango cha
maambukizi kilikuwa asilimia 3.3.
Alisema kuwa waratibu wa ngazi ya
halmashauri wamekuwa wakitoa elimu juu ya kujikinga na maambukizi ya
Ukimwi kwenye maendeleo mbalimbali ikiwemo klabu za usiku.
Alisema
kwa kuwa kondomu zinasambazwa maeneo mbalimbali yakiwemo ya starehe ni
vyema wananchi kuhakikisha wanazitumia. “Matumizi ya kondomu ni muhimu
sana kwani maeneo ya klabu za usiku na maeneo mengine ya starehe watu
wengi wanachukuana tu lakini wanakuwa hawafahamiani,“ alisema.
Alisema kuwa kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu katika Mkoa wa Dodoma hasa kipindi cha Bunge, umakini zaidi unahitajika.