skip to main |
skip to sidebar
SUGU APINGA UWANJA WA NDEGE WA SONGWE KUITWA "JAKAYA KIKWETE"
MBUNGE
wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA) amesema haungi mkono
pendekezo la Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mbeya kutaka kuuita Uwanja wa
Ndege wa Songwe jina la Rais Jakaya Kikwete.
Akizungumza na
Tanzania Daima jana jijini Dar es Salaam, Mbilinyi maarufu kama Sugu
alisema mapendekezo hayo yametolewa na watu wenye kutaka kujipendekeza
kwa mkuu wa nchi badala ya kufikiria kuutangaza Mkoa wa Mbeya katika
nyanja ya kimataifa.
Alisema Mbeya ina historia ya kutaka kujitangaza
kimataifa na uwanja huo ni fursa pekee ya kufikia malengo hayo
aliyoeleza kuwa yanataka kufifishwa na wateule wa rais.
“Siungi mkono
uwanja kuitwa kwa jina la JK, tunataka jina litakaloasisi uhalisia wa
Mbeya nasi tufahamike kimataifa, kamati ya ushauri ya mkoa chini ya Mkuu
wa Wilaya ya Mbeya mjini, Norman Sigala ilikurupuka kuleta wazo hilo
kabla ya kuwasiliana na wabunge,” alisema.
Alisema hatua hiyo ya
Sigala haiwakilishi mawazo ya wananchi bali inawakilisha mawazo ya mtu
aliyeteuliwa na kwamba wao wakiwa wawakilishi wa Mkoa wa Mbeya kwa
ridhaa ya wananchi hawawezi kukubaliana na suala hilo.
Kauli ya Sugu
iliungwa mkono na wabunge wengine wa Mkoa wa Mbeya, ambapo Mchungaji
Lukson Mwanjale wa Mbeya Vijijini (CCM) alisema anasikitishwa na hatua
hiyo ya kuliwasilisha wazo hilo bila ya kuwashirikisha wabunge.
Alisema
wakati wa kikao cha kamati ya ushauri wabunge wengi hawakuwepo na
taarifa hizo walizisikia baada ya kusoma kwenye vyombo vya habari.
Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo ambaye pia ni
mbunge wa Songwe, aliomba apewe muda wa kutaka kujua sababu zilizoibua
wazo hilo.
Wazo la kuuita Uwanja wa Ndege wa Songwe jina la Rais
Jakaya Kikwete linazidi kupata upinzani ambapo awali chama cha
NCCR-Mageuzi na kile cha PPT Maendeleo kupitia kwa viongozi wa Mkoa wa
Mbeya vilipinga wazo hilo.