Habari za msiba wake zilianza kuenea na kusambaa kama moto wa nyika usiku wa Ijumaa tarehe 7 mwaka 2012.Kila aliyepata taarifa hakuamini. Ilikuwa ni kama ndoto au jinamizi tu ambalo baada ya muda litapita na kila kitu kitakuwa sawa.
Kulipokucha,taarifa ambazo zilianza kama uvumi na kutoaminiwa na wengi, zikaanza kuthibitishwa na watu mbalimbali hususani waliokuwa naye karibu usiku ule.Uvumi ukawa ukweli. Steven Charles Kanumba akawa ameiaga dunia tarehe 7 April, 2012 akiwa na umri mdogo tu wa miaka 28 (Steven alizaliwa tarehe 8 Januari mwaka 1984 mkoani Shinyanga) .Kifo chake kikaacha huzuni na majonzi makubwa hususani kwa mashabiki wake na wa filamu ndani na nje ya Tanzania wakiwa hawaamini na kulia kwa uchungu usio kifani.
Kilichofanya taarifa za kufikwa na mauti kwa Steven Kanumba kuwa ngumu kuingia akilini mwa watu zinatokana na ukweli kwamba wengi walikuwa wamemuona jana yake na wengi walikuwa wamewasiliana naye. Kanumba alikuwa mtu wa watu. Aliongea na kila mtu na bila shaka ndio maana alipendwa na wengi. Aliwathamini mashabiki wake na hata wale ambao hawakuwa mashabiki wake. Iweje uniambia Kanumba amefariki? Nini kimetokea?Wengi walihoji kwa masikitiko.
Taratibu nchi nzima ikaanza kupata taarifa na uthibitisho. Vyombo vya habari hususani redio zikaanza kuwasaidia wananchi kuomboleza. Nyimbo za maombolezo zikatawala na huku takribani kila redio ikibadili ratiba ya vipindi vyake ili kwenda sambamba na tukio zito lililokuwa limetokea; msiba wa msanii mahiri wa filamu, Steven Charles Kanumba.
Siku tatu baadae, mazishi ya Steven Kanumba yalifanyika.Umati mkubwa wa watu ambao haukurajiwa na yeyote ikiwemo kamati ya mazishi yake, ukajitokeza kumuaga mpendwa wao. Viwanja vya Leaders pale Kinondoni vikarindima na vilio. Watu wakazimia na wengine wengi kushindwa kujua wafanyeje. Ni picha ambayo mpaka leo hii haijatoka vichwani mwa watu waliohudhuria.
Leo hii, mwaka mmoja baadae, tunamkumbuka Steven Charles Kanumba. Yeye alithubutu pale ambapo wengi walidhani hapawezekani. Alijaribu kwa nguvu na akili zake zote kuitoa sanaa ya filamu katika mipaka ya Tanzania.Alifanikiwa. Alipofariki salamu za rambirambi zilitoka kila kona ya Afrika. Waghana walimlilia.Wanigeria walibubujikwa na machozi…Wakenya walilia…kila kona ya bara la Afrika walimlilia.
Kanumba alikuwa msikivu na mwepesi wa kujifunza. Maringo aliyokuwa nayo ni ya kibinadamu. Ni yale ya kujikubali mwenyewe kwanza ili wengine nao waanze kukukubali. Alitambua wazi umuhimu wa mashabiki na watizamaji wa filamu. Alithamini mchango wao kwa vitendo. Yeye ni miongoni mwa wasanii waliojitolea sana katika shughuli za kijamii. Alichangia na kuhamasisha.
Mwaka mmoja baadae; tunamuezi vipi? Endelea kupumzika kwa amani Steven Kanumba.