Pages

Wednesday, February 13, 2013

MTWARA MAMBO SI SHWARI KWA MARA NYINGINE


 maandamano dhidi ya gesi asilia ya Msimbati mkoani Mtwara.

VURUGU za kupinga ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam uliotulia kwa takriban wiki mbili sasa, umeibuka upya.

Vurugu hizo ziliibuka upya juzi baada ya jengo la Ofisi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kata ya Majengo Mtwara Mjini, kuchomwa moto usiku wa kuamkia juzi na kundi la watu wasiojulikana.


Habari zinasema kuwa hakukuwa na madhara makubwa ya tukio hilo kutokana na umati mkubwa wa watu kujitokeza kuzima moto huo.

Hadi moto huo unazimwa, milango na madirisha ya ofisi hiyo, ilikuwa imeteketea kabisa.

Mbali ya kuchoma jengo hilo, kundi hilo lilichoma matairi ya magari katika mitaa mbalimbali ya eneo hilo na kusababisha hofu kubwa kwa wananchi hao.

Hata hivyo uchunguzi wa gazeti hili, umebaini kuwa chanzo cha chokochoko hizo mpya ni viongozi wa muungano wa vyama vya upinzani kushindwa kuwapa wananchi majibu ya kikao chao cha siri cha hivi karibuni kati yao na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kilichofanyika kwa zaidi ya saa sita nyumbani kwake, jijini Dar es Salaam.

Habari zinasema kuwa viongozi hao waliporudi Mtwara hawakusema yaliyojiri Dar es Salaam kitendo kilichochochea fujo na kusababisha kiongozi wa msafara huo, Hamza Masudi Licheta kupigwa na wananchi wa Mtwara kwa tuhuma kuwa amewasaliti.

Hivi karibuni, viongozi wa muungano wa vyama vya TLP, NCCR Mageuzi, CHADEMA, Sau, APPT Maendeleo, DP, UDP, na ADC, walishiriki mkutano na Waziri Mkuu Pinda usiku kujadili suala la mzozo wa gesi ya Mtwara.

Haikubainika sababu hasa zilizofanya mkutano huo ufanyike usiku nyumbani kwa Waziri Mkuu na ambao haukuripotiwa na chombo chochote cha habari.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake, mwenyekiti wa umoja huo, Hamza Masudi Licheta, alisema:

“Sisi tulisafiri toka Mtwara kuja Dar es Salaam kuonana na Waziri Mkuu kwa sababu alipokuwa Mtwara aliondoka kabla hatujafikia muafaka, hatukukubali kama Waziri Mkuu alivyosema, aliondoka mapeka kuwahi Dodoma na sababu aliyotoa alipokuwa Mtwara alisema anawahi Dodoma kwa kuwa uwanja wa ndege wa Dodoma hauna taa, jambo lililomlazimu kuondoka Mtwara kwa harakaharaka.”

Alipoulizwa na gazeti hili nani aliratibu safari yao kuja Dar es Salaam alisema, “Utaratibu wetu uliratibiwa na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, na tulikuja tukafanya mkutano kuanzia saa mbili hadi saa saba usiku.”

Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa viongozi hao walisafiri toka Mtwara kuja Dar es Salaam na walilala katika nyumba ya kulala wageni inayoitwa Kisuma, iliyoko jijini Dar es Salaam.

Aliongeza: “Sisi hatukuitwa na Waziri Mkuu, sisi ndio tulitaka kuonana naye kumwambia kuwa wananchi wa Mtwara hawajamwelewa katika taarifa yake aliyotoa bungeni Dodoma, pili tulimtaka yeye aondoe ile marufuku ya mikutano ya hadhara kwani Waziri wa Mambo ya Ndani amepiga marufuku mikutano yote ya hadhara huko na sasa tunashindwa kuwaelimisha wananchi kuhusu suala hilo na kadiri wananchi wanavyokosa taarifa ndio hali inazidi kuwa mbaya sasa wananchi wameanza kutupiga na kututuhumu kuwa tumehongwa kwa kuwa hatuwezi kufanya mikutano kuelezea kilichotokea katika mkutano tuliofanya usiku nyumbani kwa Pinda Dar es Salaam.”

Hamza aliongeza, “Tumeenda kwa Waziri Mkuu ili kumwambia kuwa hatumtaki mkuu wa mkoa, hata kama aliomba radhi, sisi wananchi wa Mtwara hatuko tayari kufanya naye kazi, hatutampa ushirikiano, hivyo tulitegemea kuwa Waziri Mkuu angemwambia Rais, na kesho (leo) tumeambiwa Balozi wa Nigeria nchini anakuja Mtwara, hivyo hatutaki aandamane na mkuu wa mkoa.

Alipoulizwa nani aliwalipia gharama za safari toka Mtwara kuja Dar es Salaam na kurudi pamoja na malazi, alisema: “Huwa tuna utaratibu wa kuomba wananchi, hivyo tuna mfuko wa muungano wa vyama vya upinzani.”

Hata hivyo uchunguzi wa gazeti hili, umebaini kuwa kauli ya Waziri Mkuu kuwa wananchi wa Mtwara wameelewa suala la gesi kupitia viongozi wao imeongeza utata kutokana na mkutano huo wa usiku na viongozi wa vyama vya siasa.

Mwanasiasa mmoja maarufu nchini ambaye hakutaka kutajwa jina amehoji, “Kama Waziri Mkuu alieleweka Mtwara, kikao cha usiku na viongozi wa vyama vya upinzani ulikuwa wa nini? Kulikuwa na kitu gani cha kujadili kwa siri hadi viongozi waliporudi Mtwara hawakutoa taarifa kwa wananchi?”

Taarifa ya Waziri Mkuu aliyoitoa Bungeni, Januari 31, 2013 ilionyesha kuwa amefanikiwa kumaliza mgogoro wa gesi Mtwara, kitendo ambacho kilisifiwa na wananchi wengi akiwemo Rais Jakaya Kikwete.

Wakati akitoa taarifa Bungeni, Pinda alisema kuwa amekutana na makundi mbalimbali Mtwara na baada ya kufanya nao mazungumzo, wamemuelewa na kuacha vurugu.

“Mheshimiwa Spika, kama utakavyoona, kiwango cha vurugu na uharibifu wa mali za serikali na raia kilikuwa kikubwa. Kufuatia hali hiyo, Januari 27, 2013, nililazimika kukatisha safari yangu ya kuja Bungeni Dodoma na kwenda mkoani Mtwara,” alisema.
Kwa mujibu wa Pinda, lengo la ziara yake ilikuwa kujionea hali halisi ya ulinzi na Usalama mkoani Mtwara, kupata taarifa rasmi za matukio mbalimbali yaliyotokea katika siku za hivi karibuni mkoani humo.